Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Baadhi ya wawakilishi wadi kaunti ya Nakuru wameishtumu idara ya utendakazi ya kaunti hiyo kwa kutolipa wanakandarasi mamilioni ya pesa wanazodai.

Mwenyekiti wa kamati ya utekelezwaji katika bunge la kaunti ya Nakuru Simon Wanyoike amesema kuwa baadhi ya miradi muhimu huenda ikasambaratika kutokana na kizuizi kuwa miradi hiyo ilikuwa ya mwaka wa kifedha 2014-2015.

Akiungwa mkono na wanakandarasi hao, MCA huyo wa wadi ya Lakeview alisema kuwa wanaowakilisha kamati hiyo hawajui sababu ya kutolipwa kwa madeni hayo licha ya bunge la kaunti kuidhinisha malipo hayo.

Akizungumza mjini Naivasha Jumatatu, Wanyoike alishtumu idara ya fedha kwa kukosa kueleza kwa nini madeni hayo hayakulipwa.

Aliyekuwa kiongozi wa wengi katika bunge hilo Samwel Waithuki alisema kuwa tatizo hilo litafichuliwa hivi karibuni.

“Wajenzi wa barabara hawajalipwa pesa zao na hatuna uhakika ambaye tunaweza kumuuliza kuhusiana na kutolipwa kwao,” alisema Waithuki.

Aliongeza kuwa barabara nyingi ziliharibiwa na mvua mwaka jana na zinahitaji ukarabati.

Mkazi mmoja Anthony Robi alisema kuwa mifereji ya maji taka imeharibika huku barabara nyingi zikiwa hazipitiki kutokana na ubovu.