Naibu chifu kutoka eneo bunge la Kitutu Masaba amepata uungwaji mkono siku chache tu baada ya kuwawekea faini ya shillingi elfu tano kwa watu watakaopatikana wakinywa vileo kabla ya masaa rasmi yaliyowekwa na serikali ya kitaifa.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akiongea siku ya Jumatatu, mwakilishi wa wadi ya Gesima Ken Atuti alisema kuwa sharti hilo litasaidia pakubwa watu kujihusisha na shughuli za kuwastawisha kimaisha. 

"Sioni ubaya ikiwa itamaanisha kuwa sharti watu walipe faini ili wasivunje sheria kwa maana tunahitaji watu wetu wajihusishe na shughuli za kuwainua kiuchumi badala ya kunywa vileo kwa wakati ambao sio halali," alisema Atuti.

Akiunga mkono matamshi ya Atuti, mwakilishi wa wadi ya Nyansiongo Jackson Mogusu alisema kuwa inafaa serikali iwape nguvu machifu kupambana na wamiliki wa baa wasiotii sheria.

"Nafikiria kuwa serikali inastahili kuwapa nguvu machifu na manaibu wao ili kupambana na wamiliki wa baa wanaouzia wananchi pombe kabla ya wakati uliowekwa na serikali kufika hata kama itamaanisha kufutilia mbali leseni zao za kuhudumu na wale watakaopatikana wakinywa vileo kabla ya wakati maalum wapewe adhabu kali kwa mujibu wa sheria," aliongezea Mogusu.

Chifu huyo, Sambu Bosire, aliibua tetesi kali baada yake kuagiza walevi kupigwa faini ya shillingi elfu tano, na kisha kuripoti kwenye afisi yake ili kupewa kazi za sulubu.