Share news tips with us here at Hivisasa

Wazazi wenye wanafunzi katika shule mbali mbali za upili kwenye wadi ya Bahati wamepongeza utendakazi wa mwakilishi wao wa wadi pamoja na serikali ya kaunti hiyo chini ya Gavana Kinuthia Mbugua kutokana na utoaji wa basari unaozingatia haki na usawa.

Wakizungumza Jumanne baada ya mwakilishi wa wadi hiyo Peter Nderitu kuwapa hundi ya pesa za basari kutoka kwa serikali ya kaunti ya Nakuru katika shule ya upili ya St Josephs Kirima, wazazi hao walielezea kuridhishwa kwao na namna pesa hizo zilivyogawa miongoni mwa wasiojiweza, hata licha ya kuzisubiri kwa takriban miezi saba.

“Mimi sijapata kuskia jina la mtoto wangu likitajwa kwenye orodha ya waliopewa basari, lakini nafurahia kwa sababu pesa hizo zitasaidia kuinua masomo ya wanafunzi wa shule yetu,” alisema Margaret Nyakundi.

Naye mzee Jackson Kamau alipendekeza serikali ya kaunti kuongeza mgao wake wa fedha za basari kwenye bajeti ya kila mwaka wa kifedha.

“Hatuna mashamba tena ya kugawia watoto wetu, lakini tukiwapa elimu watajinunulia ardhi. Kwa hivyo nashukuru gavana Mbugua, na kumchangamoto aongeze pesa hizo, ili watoto wetu waache kufukuzwa shuleni,” alisema.

Shule hiyo ilipata shilingi elfu 118 kufadhili masomo ya wanafunzi 59, ile ya JM Kariuki ikapata elfu mia moja na tano, St Francis Chania ikapata mgao wa shilingi elfu 68, King David ikapata mgao wa shilingi elfu 18,500, nayo shule ya upili ya Ronens ikapata elfu 18.

Ronens ni shule ya kibinafsi.

Mwakilishi huyo wa wadi alisema kwamba kama wawakilishi wa wadi katika bunge la Nakuru wanatia msukumo kwa serikali yao kufadhili wanafunzi wengi iwezekanavyo kimasomo.