Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Huku shule zikitarajiwa kufunguliwa hii leo, Jumatatu kwa muhula wa kwanza, huenda wazazi wengi wakalazimika kusalia na wanao nyumbani kufuatia kupanda kwa bei ya vitabu.

Wengi wao wanadai kuwa huenda wakalemewa kuwapa wanao haki yao ya kimsingi kwani hawawezi kumudu bei ghali ya vitabu inayoshuhudiwa kwa sasa katika baadhi ya maduka ya kuuzia vitabu mjini Mombasa.

"Maisha yamekuwa magumu kwa sasa, unajiuliza ni kitabu utamnunulia mtoto ama ni chakula. Tunaomba wenye maduka watupunguzie bei ya vitabu angalau watoto wetu wasome,’’ alisema mmoja wa wazazi.

Baadhi ya wenye maduka waliozungumza na mwandishi huyu pia walithibitisha hali hiyo, huku wakikadiria kushuka kwa mapato kutokana na idadi ndogo ya wanaojitokeza kuulizia bidhaa hiyo licha ya kuwa shule ziko karibu kufunguliwa kwa muhula wa kwanza.

Hali hii inajiri siku chache tu baada ya muungano wa wenye maduka ya kuuzia vitabu mjini Mombasa, kutangaza kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo kutokana na ughali wa hali ya maisha nchini.

Wanafunzi kote nchini wanatarajiwa kurejea shuleni wiki ijayo kwa muula wa kwanza wa mwaka 2016.