Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wazazi kutoka Kaunti ya Mombasa wamewapongeza walimu pamoja na wanafunzi waliofanya mtihani mwaka huu, kwa kuiweka kaunti hiyo kwenye ramani ya taifa kwa kutokuwa na visa vya udanganyifu kinyume na miaka ya nyuma.

Kulingana na Philes Kengo, ambaye ni moja wa viongozi wa wazazi katika eneo la Likoni, ni wazi kwamba walimu pamoja na wanafunzi katika kaunti hiyo walijikakamua vilivyo na kujiepusha na visa ambavyo ni kinyume na utaratibu wa baraza la mitihani nchini, na kuwataka washikadau kuweka juhudi ili kuendelea kuboresha viwango vya elimu katika eneo zima la Pwani.

“Tunawapongeza sana wanafunzi wetu, pamoja na walimu kwa kuwajibikia kazi zao na kufanya kaunti zetu, hasa Kaunti ya Mombasa kuepuka visa vya wanafunzi kukosa alama zao kwa sababu ya kudanganya, na ni heko kwa kila mmoja ambaye alichangia kufanikisha matokeo hayo,” alihoji Kengo.

Mtihani wa taifa wa darasa la nane ulitolewa siku ya Jumatano, huku kaunti kumi na moja zikikosa kuwa katika orodha ya zile zilikuwa na visa vya udanganyifu kwenye mtihani ulikuwa na watahiniwa 937,000.

caption: Wanafunzi wakisherehekea mitihani ya darasa la nane Mombasa. Wazazi kwenye kaunti wamepongeza walimu kwa matokeo mazuri.