Share news tips with us here at Hivisasa

Wazazi mjini Nakuru wamewataka wauzaji vitabu kuwa na huruma na ubinadamu na kujiepusha na tabia ya kupandisha bei ya vitabu maradufu haswa msimu huu ambapo wanafunzi wa kidato cha kwanza wanaripoti shuleni.

Wakiongea Jumatano mjini Nakuru wazazi wamelalamikia bei ya juu ya vitabu vya kusoma na kuwalaumu wauzaji kwa kuwakandamiza.

Rosbel Mweri ambaye ni mzazi wa watoto wawili wanaojiunga na shule ya wasichana ya Nakuru amesema kuwa bei ya juu ya vitabu inawaongezea wazazi mzigo na kuyafanya mambo yawe magumu.

“Mzazi kama mimi nina watoto wawili wanojiunga na kidato cha kwanza na inaumiza kuja hapa na kupata bei ya vitabu imepandishwa mara mbili. Wauzaji wa vitabu wanapaswa kujua kuwa tuna mahitaji mengine na wasifurahie huku wengine wakiumia,” alisema Mweri.

“Hata kama ni kupandisha bei si lazima iwe mara mbili ya bei ya kawaida,” aliongeza.

Agnes Nderitu mzazi ambaye mwanawe anajiunga na shule ya vijana ya Njoro alisema kuwa inasikitisha kuona kuwa bei ya vitabu inazidi kupanda tu wakati shule zinapofunguliwa ama pale wanafunzi wa kidato cha kwanza wanaporipoti shuleni.

“Kwanini kila wakati wanafunzi wanaporudi shule ndipo bei hupanda?” aliuliza.

Lakini kwa upande wao wauzaji wa vitabu wamejitetea wakisema kuwa ushuru wa juu unaoitishwa na serikali umewafanya kupandisha bei ya vitabu.

Denlson Mwangi ambaye ni muuzaji vitabu mjini Nakuru amesema kuwa serikaii ndiyo ya kulaumiwa kwa bei ya juu ya vitabu.

“Kile watu hawajui ni kuwa ushuru unaotozwa mali ghafi ya kuchapisha vitabu uko juu sana na lazima kila mtu atengeneze faida na hiyo inafanya bei ya vitabu kupanda,” alisema Mwangi.