Kulikuwa na kisanga katika kijiji cha Gatamaiyu mjini Naivasha Jumanne, baada ya wazazi kuvamia shule moja ya msingi eneo hilo na kuwatoa watoto wao wakilalamikia matokeo duni.
Wazazi wenye watoto katika shule ya msingi ya Kangari walivamia shule hiyo wakisema hawangevumilia tena kushuhudia watoto wao wakiendelea kufanya vibaya kwenye mitihani ya kitaifa kutokana na kuzembea kwa waalimu.
Aidha wazazi hao wenye gadhabu walimfurusha mwalimu mkuu wa shule hiyo John Njuguna pamoja na waalimu wengine, huku shule ikibakia mahame.
“Tumekuwa tukishirikiana na waalimu na kutoa kila tunapoitishwa lakini hatuoni matunda ya juhudi tunazotia kwa sababu waalimu ni wazembe,” alisema mzazi mmoja.
Alisema kwenye matokeo ya mtihani wa mwaka jana, mwanafunzi bora alikuwa na alama 285 huku wengine 20 wakiwa na chini ya alama ya mia moja.
Afisa mmoja kutoka idara ya elimu wilayani Naivasha ambaye aliomba kubanwa jina kwa misingi ya kutoruhusiwa kuongea na vyombo vya habari alisema tayari shule hiyo inafanyiwa uchunguzi wa kubaini kiini cha matokeo mabaya.
Sasa wametaka serikali kuwahamisha waalimu wote shuleni humo huku wakiapa ikiwa hilo halitafanyika, basi hawatakubali watoto wao kurejea kwenye shule hiyo.