Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wazazi ambao wanao walifanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane mwaka wa 2015 wametakiwa kuhakikisha kwamba shule za upili watakazopeleka wanao zinazingatia maadili mema kando na elimu bora.

Wito huo umetolewa na mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Christ The King mjini Nakuru mtawa Niceta Munyi.

Akizungumza kwenye mahojiano na wanahabari katika shule hiyo hapo baada ya shule hiyo kufahamishwa kuwa mwanafunzi aliyeibuka bora katika shule hiyo kwenye mtihani huo kwa jina la Stacey Kemboi alipata alama 440, Munyi aaliwahimiza wazazi kuzingatia maswala muhimu kama vile yale ya kinidhamu kabla ya kuwasajili watoto wao katika shule yoyote ile ya upili.

"Ningependa kuwahimiza wazazi waweze kuhakikisha kwamba wanapeleka watoto wao katika shule ambazo wanapata mafunzo mema na zile ambazo zinazingatia maadili mema na nidhamu ya hali ya juu," alisema Munyi.

"Wanafaa kuhakikisha kwamba wanawapeleka wanao katika shule ambazo watafanikiwa kuibuka bora baada ya masomo yao ya shule ya upili," aliongeza.

Kwa upande wake naibu mwalimu mkuu wa shule hiyo ya msingi ya Christ the King Nakuru Stephen Kimani, ambaye pia alizungumza na wanahabari aliwahimiza watakaojiunga na shule za upili kutia bidii masomoni.

Amezidi kukariri kwamba hata wale walio na talanta mbalimbali wanazidi kujibidiisha kupata elimu kwani maisha ya sasa yanahitaji waliosoma.

"Watakaojiunga na sekondari wanafaa kutia bidii kwa sababu maisha ya sasa yanategemea sana masomo. Hata wale walio na talanta mbalimbali wanaendelea na masomo yao," alidokeza Kimani.