Serikali ya kitaifa kupitia hazina ya uendelezaji maeneo bunge CDF, imetakiwa kuanzisha mpango wa kuwapa wanafunzi wa shule za chekechea na msingi chakula cha mchana, kwa lengo la kuimarisha elimu.
Wakizungumza na mwandishi huyu, baadhi ya wazazi wa shule mbali mbali katika kaunti ndogo ya Rongai jimbo la Nakuru, walisema kwamba wanafunzi huchukua muda mrefu kwenda nyumbani kupata chakula cha mchana, jambo ambalo huadhiri pakubwa wanafunzi kutoka familia maskini.
“Mwaka jana kulikuwa na kiangazi cha muda na mazao yetu yalikauka, ama kuadhiriwa na magonjwa. Japo El-nino ilileta nafuu kiasi, bado hatuna chakula cha kutosha kuwalisha hawa watoto. Shule vile vile ziko mbali na makaazi yetu, kwa hivyo mtoto wa chekechea, darasa la kwanza hadi la tatu kutembea hadi nyumbani kutafuta chakula ni kama mateso,” alisema Jonathan Kimeto.
Mzazi mmoja mwenye wanafunzi katika shule ya msingi ya Athinai kwa jina Winnie Jerop alisema kuwa, kwa watoto kurejea shuleni bila ya kula chochote, jambo ambalo huwafanya kutomakinika madarasani.
“Hata wakija nyumbani na wale, safari ndefu anayotembea inamfanya akifika shuleni amehisi njaa tayari, na hivyo kuadhiri masomo yake. Familia nyingi hazina uwezo wa kuwapa chakula cha kubeba shuleni, serikali itusaidie kuwapa chakula,” alisema Winnie.
Naye Geoffrey Kamau kutoka shule ya msingi ya Kampi ya moto akadokeza kwamba, kuwapa wanafunzi chakula cha mchana shuleni, kutawaleta watoto wote pamoja kutoka jamii tofauti.