Wazazi wa Kaunti ya Mombasa wamekosolewa kwa kuchangia kwa watoto wao kuacha masomo na kujihusisha na maswala ya uhalifu.
Akiongea mjini Mombasa siku ya Jumamosi katika mkutano wa usalama, Naibu Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Mahmoud Salim alisema kwamba watoto wengi wadogo wamesalia majumbani bila kwenda shuleni hali inayowasukuma katika harakati za uhalifu.
Afisa huyo tawala alisema kwamba hali hiyo imeshuhudiwa katika maeneo ya Old Town, Majengo na Kisauni ambapo vijana wadogo wa miaka 12 wamejiunga na makundi ya kihalifu.
Alihoji kwamba chanzo kikuu cha masaibu hayo ni wazazi wenyewe wa watoto hao kukosa kuchukua hatua za dharura kuwaepusha na uhalifu.
“Wazazi lazima kuwaachilia watoto wao kwenda shuleni na kujiepusha na maswala ya uhalifu kwani wengi wa wazazi wamechangia watoto wao kujisukuma na uhalifu hali ambayo imehatarisha maisha ya wakazi wengi Mombasa," alisema Salim.
Bw Salim aliwahimiza wazazi kuhakikisha kwamba watoto wao wanahudhuria masomo shuleni ili kuweka msingi bora wa maisha yao na akawaonya wazazi wasiyowapeleka watoto wao shuleni kwamba wataadhibiwa.
“Tunawaomba wazazi tafadhili hakikisheni watoto wenu mnawapeleka shuleni ili kuzuia watoto hawa kujiunga na maswala ya uhalifu na kuwa tishio kwa usalama wa wakaazi," aliongeza Salim.