Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Lamu Shakillah Abdallah amewatahadharisha wazazi wanaowanyima watoto wa kike elimu kwamba wataadhibiwa kisheria.

Akizungumza katika kongamano la elimu lililowajumuisha viongozi mbalimbali wa sekta hiyo pamoja na wazazi katika ukumbi wa kiswahili mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Shakillah alisema kwamba inasikitisha kuwaona baadhi ya wazazi wakiwatelekeza watoto wa kike katika maswala ya elimu.

Kulingana na Shakillah, ni lazima mtoto wa kike apewe elimu inayostahili sambamba na mtoto wa kiume, na swala la elimu halipaswi kuegemea upande wa wanaume pekee.

Aidha, alitaja maeneo ya kisiwani Lamu, Kinango kaunti ya Kwale, Kadzandani kaunti ya Mombasa kuwa maeneo yanayowatelekeza watoto wa kike.

Shakillah alisema kwamba itikadi ya kale ya kumpatia nafasi mtoto wa kiume elimu na kumbagua yule ya kike ilipitwa na wakati, na hatua hiyo huenda ikarudisha nyuma kimaendeleo kaunti za pwani.

“Kuna baadhi ya wazazi bado wako na itikadi za kale za kuwatelekeza watoto wa kike katika maswala ya elimu, wakati huo umepita na sasa lazima kila mtoto apate elimu ndio kesho aweze kutusaidia sisi wazazi,” alisema Shakillah.

Ameitaka jamii kuwaripoti wazazi wanaowaoza mapema mabinti zao badala ya kuwapatia elimu ili wazazi hao sambamba na wale wanaowaoa watoto wadogo waadhibiwe kikamilifu.

Kiongozi huyo ameahidi kushirikiana na serikali za kaunti za pwani ili kuona kwamba mpango wa kuwafadhili wanafunzi masomoni unaimarishwa zaidi ili waweke msingi bora maishani.