Share news tips with us here at Hivisasa

Mchungaji wa chuo kikuu cha Kisii kasisi Lawrence Nyaanga amewaomba wazazi wote katika Kaunti ya Kisii kuwa waangalifu kwa watoto wao ambao wameacha shule na kujihusisha na vitendo visivyo na msingi wowote ili kuwachukulia hatua.

Kulingana na Nyaanga, baadhi ya watoto ambao ni wanafunzi wa baadhi ya shule katika kaunti hiyo wameacha shule na kujiunga na dini inayoshukiwa kuwa ya ushetani, huku wakiahidiwa kununuliwa magari, majumba na kupewa pesa, jambo ambalo limesababisha baadhi ya wanafunzi kuacha masomo na kujiunga na dini hiyo mjini Kisii.

Nyaanga alisema wao kama makasisi wamekuwa wakipata ripoti hizo kwa muda mrefu, huku wakiomba wazazi kuwafuatilia wanao kwa mienendo ili kuwabadilisha tabia na kuwachukulia hatua ili kuwazuia kutojihusisha na dini hizo za ushetani.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano mjini Kisii, Nyaanga aliomba wazazi kuwa waangalifu kwa wanao ili wasije kujiuliza masuala mengi baada ya wanao kujiunga na dini hizo zinazoshukiwa kuwa za ushetani wakitafuta mali ambayo si halali.

“Naomba wazazi wote katika kaunti yetu kuwa waangalifu na kuwafuatilia wanao kwani imeripotiwa kwetu sisi wachungaji kuwa kuna baadhi ya wanafunzi wameacha shule na kujiunga na dini ya ushetani wakiahidiwa mali,” alisema Nyaanga.

Aidha, Nyaanga aliwaomba maafisa wa polisi kuanzisha uchunguzi kuhusiana na jambo hilo ili kuwaokoa watoto wanaoacha shule na kujihusisha na vitendo vya aina hiyo visivyo na msingi wowote.