Wazazi kote nchini wameshauriwa kuwa waangalifu na kuwalinda watoto wao dhidi ya kujihusisha na vitendo vya uhalifu.
Wito huo ulitolewa baada ya kubainika kuwa idadi kubwa ya watoto wanajihusisha na vitendo vya uhalifu.
Akizungumza siku ya Jumapili katika kanisa la kikatoliki mjini kisii askofu Joseph Mairura aliwahimiza wazazi kuwalinda watoto wao kwa kuhakikisha hawashiriki vitendo vya kihalifu.
“Naomba kila mzazi nchini awe mwangalifu kwa mtoto wake ili wasijihusishe na vitendo vya uhalifu,” Mairura alisema.
“Mtoto anapojiunga na kundi lolote la uhalifu siku zake huwa fupi maishani na ninaomba kila mzazi kumfunza mtoto wake tabia bora na jinsi ya kuishi bila kujihusisha na vitendo vya aina hiyo,” aliongeza Mairura
Wakati huo huo, askofu huyo alipongeza Rais Uhuru Kenyatta kwa kupambana na uhalifu nchini na kuwataka wakenya kuungana pamoja kuombea Kenya.
“Naomba tuombee viongozi wote ili wafanye yale wanastahili kuyafanya. Maombi ndio mwongozo wa kila jambo maishani,” askofu huyo alisema.