Mkurugenzi wa maswala ya watoto katika kaunti ya Nyamira Samuel Masese amewatahadharisha wazazi pamoja na walezi dhidi ya dhulma kwa watoto, akisema kuwa hiyo ni kukiuka sheria iliyoko ya kuwalinda watoto.
Hayo yamejiri kufuatia visa vingi ambavyo vimeendelea kukithiri vya wazazi na walezi ambao huwashambulia kinyama watoto wao, kuwatelekeza na pia kuwafanyisha kazi ngumu haswa wakati huu wa likizo kinyume cha sheria.
Masese amesema kuwa kuna sheria inayowalinda na pia kutetea haki zao, na watakaopatikana wakivunja sheria watachukuliwa hatua kali.
"Afisi yangu imepokea visa vingi vya wazazi pamoja na walezi ambao wameendelea kuwadhulumu watoto na ni vyema wajue kuwa sheria iko na watatiwa mbaroni na kushtakiwa," alisema Masese.
"Tumewaokoa baadhi ya watoto kutoka mikononi mwa wazazi wakatili na wengine wako kwenye nyumba za watoto mayatima kwa usalama wao," aliongezea Masese.
Ni hivi maajuzi mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 35 alihukumiwa kifungo cha miaka sita gerezani na mahakama ya mji wa Keroka baada ya kupatikana na kosa la kumtesa na kumshambulia visivyo mpwa wake mvulana mwenye umri wa miaka sita na kumwachia majeraha mabaya mwilini.