Wazazi walio na watoto wasio na uwezo wa kuongea na kusikia katika Kaunti ya Kisii wameshauriwa kutowaficha wanao nyumbani, ila kuwapeleka wanao shuleni ili kupokea mafunzo yao kama watoto wengine.
Hii ni baada ya kubainika kuwa idadi kubwa ya wazazi katika kaunti ya Kisii ambao wana watoto wa aina hiyo hawawapeleki watoto hao shuleni, jambo ambalo limekashfiwa kwa asilimia kubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari mnamo siku ya Jumatano katika shule ya msingi ya Kisii, mwalimu anayesimamia watoto hao Pamela Bosire, wazazi wengi ambao watoto wao hawaongei wala kusikia huwaficha nyumbani, huku akisema hilo haliwezi kusaidia.
“Wazazi wengi wanapoona mtoto hana uwezo wa kusikia na kuongea husema mtoto huyo ni mwenda wazimu, naomba wazazi wale wako na watoto wa aina hiyo waletwe kwa shule hii ili waweze kufundishwa na kuonyeshwa jinsi ya kuishi katika jamii,” alisema Bosire.
“Hakuna haja kwa wazazi kunyima watoto wa aina hiyo haki zao za masomo na haki zingine lazima kila binadamu ashughulikiwe sawia na wengine,” aliongeza Bosire.