Share news tips with us here at Hivisasa

Wakaazi wa kaunti ya Mombasa wametahadharishwa kuwachunga watoto wao kutokana na kujiunga na makundi ya kigaidi yanayolenga vijana wadogo walio shuleni.

Kulingana na kiongozi wa vijana katika eneo la Kisauni mjini Mombasa Maxwell Masai, idadi kubwa ya vijana wanaojiunga na kundi ya kigaidi la Alshabab ni vijana wa shule za msingi, upili na vyuo vikuu, hali ambayo imechangia hofu ya usalama katika kaunti hiyo.

Akiongea mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Masai alisema kwamba lazima kwa wazazi na jamii kwa kujitolea kimasaomaso na kuwashauri vijana wao kuhusu athari za kujiunga na makundi ya kigaidi kwani kundi la Alshabab linalenga vijana wa umri mdogo.

“Tunawaomba wazazi na jamii kwa jumla kuwa makina na watoto wao kwani taarifa ambazo idara za usalama zimesema huenda vijana wengi ambao bado wako mashuleni wakaangamiza kutokana na kusajiliwa na kundi hiyo la kigaidi,” alisema Masai.

Kiongozi huyo wa vijana amezidi kuwarai vijana katika kaunti ya Mombasa kuzingatia msingi wa maisha yao pamoja na kuwa watu wenye maadili mema ili kuona kwamba usalama unadhibitiwa.

Aidha, ameahidi kufanya mikutano ya baraza ya vijana katika kaunti hiyo ili kuona kwamba vijana wanaokolewa kutokana na kujiunga na kundi la kigaidi la Alshabab.