Wazee na viongozi kutoka eneo la Kaptich katika kaunti ya Uasin-Gishu wameunga mkono hatua ya tume ya kitaifa ya ardhi (NLC) kutupilia mbali vyeti vya umiliki ardhi ambavyo vimo mikononi mwa askofu wa kanisa la Katoliki Dayosisi ya Eldoret Cornelius Korir.
Wazee hao wamesisitiza kwamba vyeti hivyo ni bandia huku wakisema kwamba ardhi hiyo ya zaidi ya ekari 40 ni ya jamii ya Kaptich ambayo imetengewa ujenzi wa shule ya upili ya Kaptich.
Wakiongozwa na Abraham Kisorio walipongeza mwenyekiti wa tuume ya ardhi Mohammed Swazuri kwa kubomoa mijengo ambayo kanisa la katoliki lilikuwa limejenga katika ardhi hiyo.
Licha ya Swazuri kuumrisha kubomolewa kwa mijengo hiyo kamati ya maendeleo katika eneo hilo ilimtaka askofu Korir kujiepusha na walaghai wa ardhi Uasin-Gishu.
Wazee husika walimtaka askofu huyo kuomba jamii ya eneo hilo msamaha kwa madai ya kuwaita wakora.
"Sisi sio wakora, askofu ndiye alitumiwa na wakora mjini Eldoret kutulaghai shamba letu. Tunataka atuombe msamaha kama mtumishi wa Mungu ambaye anaelewa Bibilia na sheria ya nchi," Alisema Kisorio.
Wazee hao wamesisitiza kwamba wao ndio wako na cheti halali cha umiliki ardhi hiyo.
Walidai walipokea cheti hicho kutoka kwa mlowezi aliyekuwa akimiliki ardhi hiyo wakati wa utawala wa wakoloni.
Askofu Korir alipinga madai hayo huku akishtumu tume ya Swazuri kwa kukosa uwazi katika utendajikazi wake.
"Tume ya Swazuri ina mapendeleo. Mbona hawakutaka kusikiza upande wetu kuhusiana na umiliki wa ardhi hiyo? Ardhi hii ni ya kanisa la katoliki na tuliiipata kwa njia ya haki," alisema Korir.
Askofu Korir alisema atatumia njia ya mahakama ili kuhakikisha kwamba kanisa lake linaendelea kumiliki ardhi hiyo.