Waziri wa afya katika kaunti ya Kisii Sarah Omache amewahimiza wakazi wa kaunti hiyo kujitokeza kwa wingi kupimwa ugonjwa wa saratani kuanzia tarehe 8 mwezi ujao wa Novemba, zoezi ambalo litachukua wiki moja.
Zoezi hilo litafanyika katika hospitali ya rufaa na mafunzo ya Kisii iliyoko mjini Kisii ili kupima wakazi na kuwatibu kama njia moja ya kupunguza idadi ya wale wanaoathirika na ugonjwa huo ambao umeonekana kuwasumbua watu kwa asilimia kubwa.
Akizungumza mnamo siku ya Jumatano katika hospitali ya Rufaa ya Kisii, Omache aliomba watu kutoogopa kupimwa ila kujitokeza kuchunguzwa kimwili.
Aina za ugojwa wa saratani ambazo zitapimwa na kushughulikiwa miongoni mwao ni saratani ya matiti, saratani ya mfuko wa uzazi na saratani ya kibofu.
Imebainika kuwa katika kaunti ya Kisii, saratani ya matiti ndio imewasumbua idadi kubwa ya watu; ikiwa kwa asili mia 59 kulingana na ripoti iliyochunguzwa kwa mwaka mmoja.
“Tutakuwa na kambi ya kupima na kutibu kuanzia tarehe 8 mwezi ujao hapa Kisii, na itachukua wiki moja kukamilika. Naomba wakazi wa kaunti ya Kisii kujitokeza kwa wingi kwa shughuli hiyo ili kutibiwa,” alisema Omache.
Msimamizi wa afya katika kaunti ya Kisii Dkt Gofferey Ontomu aliwaomba wananchi kutotumia tumbaku,m pombe na chakula isiyo halali kwani husababisha mtu kuwa na saratani za aina hizo zote.