Waziri wa afya katika kaunti ya Nakuru Mungai Kabii ametoa wito kwa wakazi wa Nakuru kufika kwenye vituo vya kiafya ili kufanyiwa uchunguzi wa kubaini iwapo wana saratani, hali anayosema itapelekea mgonjwa kushughulikiwa haraka iwezekanavyo.
Akiongea na mwandishi huyu Alhamisi, Mungai alisema kuwa kupitia kufanyiwa uchunguzi huo, mtu atabaini hali yake ya kiafya, na iwapo atapatikana na ugonjwa huo kutibiwa kwa wakati.
Aliongeza kusema kuwa hospitali kuu ya mkoa wa Bonde la Ufa iliyo mjini Nakuru ina mashine za kupima iwapo mtu ana ugonjwa huo na vilevile zahanati ambazo zinaweza kushughulikia hali hiyo.
Kwa sasa saratani ya matiti, ile ya njia ya mkojo kwa wanaume na saratani ya mlango wa uzazi kwa wanawake ndizo zinazoweza kushulikiwa katika vituo hivyo kwa muujibu wa kabii.
Kwa upande wake, afisa wa afya ya umna katika kaunti ya Nakuru Dkt Sammy Mwaura katika mahojiano alisisitiza kwamba kutibiwa mapema kwa ugonjwa wa saratani kunaweza kuwa nafuu kwa mgonjwa kwani anaweza kupona kabisa.
Na ili kujikinga na ugonjwa huo, Mwaura alisema kuwa watu wanafaa kuepuka kula vyakula vyenye kemikali nyingi, unywaji wa pombe na uvutaji wa sigara miogoni mwa sababu zingine.
Huku dunia ikiadhimisha siku ya kote duniani Alhamisi hii ya tarehe 4 Februari ,imebainika kwamba watu elfu moja hapa nchini wanaishi na ugonjwa huo.
Tamati…………….