Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya kaunti ya Nakuru kupitia kwa wizara ya Teknolojia na mawasiliano imeweka mikakati ya kuhakikisha kwamba mradi wa mtandao uliozinduliwa kwenye kaunti ya Nakuru mwaka wa 2014 hauwezi kutumiwa kuangalia maeneo yaliyo na picha na video chafu.

Hakikisho hilo limetolewa na waziri Stephen Maritim, ambaye ni waziri wa teknolojia ya mawasiliano kupitia kwa mahojiano ya kipekee na mwandishi huyu siku ya Jumatano.

Aidha, alisema lengo la kuzinduliwa kwa mtandao huo maalum lilikuwa kuwasaidia watu mbalimbali kujinufaisha kama vile wanafunzi na wakulima, kwa kuwawezesha kutafuta habari muhimu kuhusiana na taaluma zao.

Aidha, amewahakikishia wakazi wa Nakuru kwamba mtandao huo maalum unafanya kazi, huku akitaja maeneo mbalimbali ambayo mitandao hiyo inapatikana kwa urahisi.

Wakati huo huo, ameangazia baadhi ya mipango waliyo nayo kama wizara wanayolenga kutekeleza hivi karibuni kama vile kuweka huduma za simu zinazotumia intaneti kuwasiliana na wafanyikazi wa wizara hiyo katika kaunti ndogo miogoni mwa mipango mingine.

Hata hivyo, amekiri kwamba fedha walizo nazo kwa sasa kwenye bajeti ya mwaka huu wa kifedha haziwezi kutosha katika utekelezaji wa baadhi ya miradi waliyo nayo kwa sasa.

Wakati huo huo, ameweka bayana kwamba wawekezaji wanakaribishwa kwenye kaunti hiyo kuwekeza kwenye teknolojia ya mawasiliano, huku akiwahakikishia kwamba serikali ya kaunti itashirikiano nao kikamilifu.

Kando na hayo, amesema kwamba wizara yake imefanikisha mradi wa ukusanyaji wa ushuru kwa kupitia njia ya kidijitali, huku akiwahimiza wakazi kulipa ushuru kwa kupitia mfumo huo.