Watu zaidi ya kumi wamejeruhiwa vibaya kufuatia makabiliano kati ya jamii mbili zinazoishi katika mpaka wa Kaunti ya Kisii na kaunti ya Narok.
Mzozo kati ya jamii hizo mbili unasemekana kuanza usiku wa Jumapili katika nyumba ya burudani eneo la Kiango Nyanthiwa. Chanzo cha mzozo huo haujabainika lakini kulingana na kamishna wa kaunti wa eneo hilo, Abdul Hakim, kuna uwezekano kuwa mzozo huo ulikuwa wa mashamba.
Vita hio ulipelekea kuchomwa kwa nyumba kadhaa na mashamba ya miwa. Watu wengi walipata majeraha huku watatu waliojeruhiwa vibaya kwa mishale wakipelekwa katika Hospitali Kuu ya Kisii. Mmoja wa watatu waliojeruhiwa vibaya ana mshale uliokwama kifuani na kulingana na daktari mkuu katika hospitali hiyo ya Kisii, anasubiri kuenda operesheni ili kutolewa mshale huo.
Aidha, Hakim aliwaongoza maafisa wa usalama hadi eneo la vita ambapo walitawanyisha wahusika na kurejesha halo ya utulivu.
''Uchunguzi umeanzishwa na maafisa wa polisi kutambua haswa kiinii cha mzozo huo na waliochangia ili wachukuliwe hatua ya kisheria kwa kuwa ni hatia kuchochea mapigano kati ya jamii," alisema Hakim.