Mamia ya wananchi walipata fursa ya kusajiliwa wakati wa ziara ya chama cha Wiper katika maeneo kadhaa ya Pwani wikendi.
Viongozi mbalimbali wa chama hicho kilicho katika muungano wa Cord waliamua kuzuru maeneo mbalimbali lengo kuu ikiwa ni kuhimiza Wapwani kujitokeza kwa wingi katika zoezi la usajili wa wapiga kura.
Viongozi hao walifanya mikutano kadhaa hasa katika vituo vinavyoendesha usajili huo na kuongea na wananchi moja kwa moja huku idadi kubwa ya wananchi waliohudhuria wakipata fursa ya kujisajili.
Siku ya Jumamosi kiongozi wa chama hicho Kalonzo Musyoka akiandamana na viongozi wengine walizuru kaunti ya Kwale na kuwahutubia wananchi juu ya zoezi hilo ambapo wananchi walijitokeza kwa wingi.
Jumapili ilikuwa zamu ya watu wa Likoni katika Kaunti ya Mombasa ambapo watu wengi walijiandikisha kama wapiga kura huku idadi kubwa iliyoshuhudiwa ikiwa ni vijana.
Akiongea katika hafla hiyo, Kalonzo alikana madai kwamba Wapwani huwa hawapigi kura akisema kuwa hiyo ni dhana ya kutaka kupotosha wananchi.
“Wale wanakaa kule Nairobi na bara wanasema kuwa watu wa Pwani hawajihusishi na mambo ya kupiga kura, lakini mimi nataka niwaambie kwamba huu ndio wakati wenu sasa,” alisema Kalonzo.
Seneta wa Mombasa Hassan Omar alisema kuwa tatizo linalowafanya Wapwani wachache kujitokeza katika zoezi la uchaguzi ni kukosa kuhamasishwa ipasavyo.
Omar alisema kuwa licha ya tume ya uchaguzi IEBC kuwasajili watu wengi mwaka wa 2012, ni watu wachache mno waliojitokeza kupiga kura.
“Katika watu milioni moja waliosajiliwa ni watu laki nane tu waliopiga kura, lakini saa hii tumelenga watu wengi zaidi na naamini kwamba sote tukijitokeza tutabadilisha mambo,” alisema Omar.
Chama cha Wiper kimesema kuwa kimechukua hatua hiyo ya kuhamasisha wananchi baada ya kugundua kwamba watu wengi hawana ufahamu wa maswala ya upigaji kura.