Wafanyabiashara wenye hoteli kubwa na maeneo ya burudani mjini Mombasa wameanza kushuhudia kuimarika kwa mapato kufuatia ongezeko la watalii wanaozidi kufurika Pwani.
Kwenye kikao na wanahabari mapema Alhamisi, mwenyekiti wa wenye hoteli na maeneo ya burudani Mombasa Sam Ikwaye alisema wanatarijia kati ya asilimia 80-90 ya vitanda vitakuwa vimelipiwa ifikapo mapema wiki ijayo.
"Tumeshuhudia idadi kubwa ya wageni tangu mwezi huu uanze, wakiwemo wageni kutoka mataifa ya nje na hata wa humu nchini. Hali ikisalia hivi, natumai ifikapo mwisho wa wiki huu vyumba vyote vitakuwa vimenyakuliwa na wageni," alisema Ikwaye.
Mwezi uliopita meli mbili; MS Nautica na MV Isgnia ziliwasili Mombasa na watalii zaidi ya elfu mbili kutoka mataifa ya Uingereza, Ujerumani, Australia, Canada, Marekani na Norway.
Mwaka uliopita idadi ndogo ya wageni ilishuhudiwa nchini kutokana na hofu ya usalama iliosababishwa na msururu wa mashambulizi yaliyotekelezwa na kundi la kigaidi la Al Shabaab katika sehemu za Nairobi na Mombasa, hali iliyopelekea Uingereza kuiwekea Kenya vikwazo vya usafiri.
Hata hivyo mabadiliko makubwa yameshuhudiwa mwaka huu kufuatia kuimarika kwa usalama.