Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Juhudi zozote za kutaka kuwaondoa wahudumu wa magari ya aina ya Tuk-Tuk kutoka katikati ya jiji la Mombasa utapingwa vikali na wenye magari hayo pamoja na vijana ambao wanahudumu kama madereva wa magari hayo.

Kulingana na wahudumu hao, serikali ya kaunti kwa kushirikiana na kamati mbali mbali za kushughulikia masuala ya utalii katika Kaunti ya Mombasa wanataka kuwanyima vijana haki halali ya kujitegemea kupitia kwenye shughuli za kuhudumu kupitia magari hayo.

Kupitia kwa Suleiman Guyo, ambaye ni mwanakamati katika chama cha wenye tuk tuk na chama cha madereva kwenye wilaya ya Kisauni, akiongea kwa niaba ya wengine aliesema kuwa kuna mpango wa baadhi ya viongozi wa kisiasa pamoja na mabwanyenye katika jiji kuu la Mombasa kufanya njama kuwafukuza jijini ili wafaidi kibiashara.

Guyo aliongeza kudai kuwa japokuwa bado suala hilo limezuka, bado wanangoja mawasiliano rasmi kutoka upande wa serikali ya kaunti ili kuwapa mwelekeo wa kisawasawa.

Aidha, ameongeza kusema kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara flani kwenye jiji hilo hasa wenye magari ya kuhudumu biashara za taksi wamewaonea kinyongo na kile wanadai kukosa wateja kwenye magari yao na wanahisi wenye tuk-tuk ndio wanasababisha kukosa wateja.

“Sisi hufanya biashara hii kila siku na tunatoza abiria hela kidogo kusafiri hadi mahali anataka kwenda, lakini sasa magari ya taksi huwatoza nauli ya juu ndo sababu wateja hupendelea tuktuk, wenye taksi wanataka tutoke kati ya jiji ndio wapate biashara,” alisema Guyo.