Wamiliki wa mabaa na vilabu mjini Nakuru wameonywa dhidi ya kuwakubalia vijana na wanafunzi walio chini ya umri wa miaka 18 kuingia katika vilabu vyao.
Mwakilishi wadi ya Biashara Stephen Kuria amesema kuwa kama viongozi watahakikisha kuwa hakuna wanafunzi wanaopatikana karibu na maeneo ya burudani kama vile vilabu na kumbi za disko wakati huu wa likizo ya krismasi.
Akizungumza ijumaa alipozindua shuguli ya vijanakusafisha mji wa Nakuru Kuria ameonya kuwa wataifunga baa ama kilabu kitakacho kiuka sharia na kuwaruhusu watoto kuingia ndani na kununua pombe ama madawa mengine ya kulevya.
“Sisi kama viongozi wa Nakuru hatutakubali wamiliki wa vilabu kufanya biashara na kuwaharibu watoto wetu msimu wa krismasi.Kila klabu ama baa ni lazima wahakikishe kuwa kila anayeingia katika maeneo yao ana kitambulisho cha kitaifa,” alisema Kuria.
“ Iwapo watakiuka hilo basi tutawaongoza wananchi kwenda kufunga vilabu hivyo na kuwashika wenyewe,” aliongeza.
Kuria aliwataka wazazi kutowapa pesa nyingi watoto wao akisema kuwa pesa hizo huwachochea watoto kwenda katika maeneo ya starehe.
“Wewe kama mzazi usimpe motto wako pesa kabla hujajua anakwenda wapi na atafanyia nini pesa unazompa kwa sababu tunapowapa pesa nyingi hapo ndipo wanaanza kufikiria mabo ya kwenda vilabuni na kununua madawa ya kulevya,” alisema Kuria.