Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kufuatia visa vya ulawiti pamoja na ubakaji kuendelea kuripotiwa katika kaunti ya Mombasa, wanawake kutoka kaunti hiyo wametaka kushirikishwa kikamilifu kwa wazazi wa waathiriwa ili kupata uchunguzi uliokamilika na kuondoa shaka miongoni mwa wazazi husika.

Wanawake hao ambao waliandamana siku ya Alhamisi wakiongozwa na kiongozi wa 'Muslim Women Alliance' Farida Rashid  walisema kuwa visa hivyo vya ulawiti na kunajisiwa kwa watoto wadogo vinaendelea kukita mizizi katika maeneo mengi nchini, na sharti uongozi husika kulishughulikia suala hilo mapema na haraka.

Walisema kuwa uhusishwaji wa wazazi wa waathiriwa ni mhimu hasa kwenye awamu na mchakato mzima wa kufanya uchunguzi kuhusiana na visa hivyo ambavyo wanadai vinatekelezwa na watu wazima na wengi wao wanakuwa jamaa wa karibu wa muhusika.

Kwa muda wa siku chache zilizopita, kumekuwa na visa vingi vya watoto wadogo kunajisiwa, huku wengi wa wahusika wakuu wakiwa ni walimu, jamaa na rafiki za waathiriwa.

Kisa cha hivi karibuni ni cha mtoto mmoja wa shule ya msingi ambaye inasemekana alinajisiwa na mwalimu wake na kumficha katika mtaa wa Mtwapa ambapo iligunduliwa baada ya zaidi ya siku 30, na bado inasubiriwa kuona kama ni hatua gani ya kisheria itachukuliwa dhidi ya mshukiwa huyo.