Share news tips with us here at Hivisasa

Wasi wasi umeghubika kikundi kimoja cha wakulima mjini Naivasha, baada ya wezi wa mifugo kuvamia vijiji vitatu na kuiba takriban mbuzi mia moja.

Wezi hao walivamia vijiji vya Mirera, Longonot na Mwiciringiri, huku ikikisiwa kuwa waliwapitisha mifugo hao kwenye mbuga ya wanyama ya Longonot bila ya kupatikana.

Uvamizi wa kwanza umefanyika eneo la Mirera ambapo zaidi ya mbuzi hamsini wameibiwa huku mkulima mmoja akiibiwa mbuzi 36, tukio ambalo limefanyika usiku wa kuamkia leo.

Na baada ya tukio hilo, wezi hao walifululiza hadi kwenye vijiji vya Longonot na Mwiciringiri vinavyopakana na kuwaiba mbuzi wengine.

Mkazi mmoja, Joel Kimani, ambaye amepoteza mbuzi kumi na tisa amesema kuwa wizi huo ulikuwa umepangwa kwani wale walioutekeleza walikuwa wakijua boma zilizo na mbuzi wengi.

“Wezi hao walituvamia majira ya saa tisa asubuhi ya leo (Jumatatu) na kutekeleza uovu huu,” Kamau alisema.

Akizungumza na mwandishi huyu, mkuu wa wilaya ya Naivasha Abraham Kemboi ameahidi kufuatilia swala hilo ili wezi hao watiwe mbaroni.

“Afisi yangu inawasiliana na maafisa wa kitengo cha kupambana na wizi wa mifugo walio na kambi yao eneo la Mirera ili msako ufanyike mara moja,” alisema Abraham.