Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wezi waliokuwa wamejihami kwa bunduki walivamia wakazi katika kituo cha kibiashara cha Heshima Engashura, wadi ya Kiamaina, Kaunti ya Nakuru na kuwapora pesa na bidhaa za kielektroniki zikiwemo simu, Jumamosi usiku.

Wezi hao ambao kulingana na wakazi wa ploti hiyo walikuwa zaidi ya watano, na walikuwa na gari ndogo jeupe ambalo walitumia kutoroka.

Yaaminika wezi hao walikuwa wamefuata mwenyeji mmoja anayeishi kwenye ploti hiyo ambaye alikuwa na gari ndogo pia majira ya saa mbili usiku. 

Huku wakiwahadaa kwa bunduki, waliwaamrisha kufungua milango na kuwapora mmoja baada ya mwingine, huku waliokataa wakipatilizwa kichapo.

Baada ya kuwahangaisha kwa muda wa dakika 45, wezi hao walimteka nyara mama mmoja kwa jina Mercy Nyokabi, ambapo walitishia kwamba wangempiga risasi iwapo wenyeji wangepiga kamsa ama kuita polisi.

Hata hivyo, wezi hao walimwachilia mama huyo na kuingia kwenye gari lao baada ya kumlazimisha kuondoka naye na kwenda umbali wa kilomita moja, wakati waliita gari lao lililokuwa limepakiwa karibu na kituo cha radio cha Sauti Ya Mwananchi.

Hata hivyo, baada ya kuachiliwa kwa mama huyo, wakaazi waliweza kuita polisi wa Bahati waliofika kwa haraka.

Tangia Disemba 25, 2015 kufikia sasa, visa vinne vinavyohusisha wizi wa kimabavu kutoka kwa watu wenye bunduki vimeshuhudiwa katika eneo bunge la Bahati, huku mtu mmoja akiuawa.

Katika mkutano wa kujadili maswala ya amani na wakaazi wa Ahero Bahati mnamo 8, Januari,2016, naibu kamishna wa kaunti ndogo ya Bahati Kithinji Ithai, alisema polisi wanefanya doria zaidi kuimarisha usalama ambao sasa umedorora mno.