Kusambaa kwa haraka kwa mmea wa gugu maji katika ziwa Naivasha kunahatarisha uvuvi na utalii kwenye ziwa hilo.
Gugu maji hilo sasa limefunika aslimia 30 ya ziwa hilo, hali ambayo imewatia hofu washikadau kwenye ziwa hilo, wakiitaka serikali ya kaunti sasa kuingilia kati.
Miezi miwili iliyopita gavana Kinuthia Mbugua alisema serikali yake ingeshirikiana na chuo kikuu cha Karatina ili kung'oa mmea huo.
Mwenyekiti wa ushirika wa wamiliki wa mashua kwenye ziwa hilo David Kilo, akiongea mnamo Jumatatu na wanahabari alisema gugu maji hilo limezidi mno katika eneo la Kamere.
Alisema kwamba neti zinazogharimu mamilioni ya pesa zimeharibika kutokana na mmea huo, huku mara kwa mara wakishindwa kupenyeza baadhi ya sehemu za ziwa.
“Maji yakiongezeka, eneo ambalo lina gugu maji pia linaendelea kupanuka, na kuharibu neti pamoja na shughuli za uvuvi,” alisema Kilo.
Hata hivyo alisema kuwa wanaunga mkono kwa dhati harakati za serikali ya kaunti ya Nakuru kukabiliana na mmea huo hatari.