Kuna haja ya kuweza kutahini maswala mbalimbali ambayo yamekuwa yakifunzwa shuleni na ambayo hayajakuwa yakifanywa kama mitihani.
Huo ni usemi wa katibu katika wizara ya elimu Belio Kipsang kupitia kwa mahojiano ya kipekee na mwandishi huyu.
Kulingana naye, maswala hayo ni kama vile ya uadilifu, maswala ya uwazi na yale ya uzalendo,huku akisema kwamba maswala hayo yatajumuishwa kama yale ambayo yanafaa kutahiniwa na pia yatajumuishwa katika mojawapo ya masomo ambayo hujumuishwa kwenye mitihani.
"Watu wengi huwa hawatilii maanani kitu chochote ambacho hakiletwi kama mtihani. Hata hivyo, huwa tunafunza baadhi ya mambo kama vile yanayohusiana na uadilifu na uzalendo na kutokana na hilo, kuna haja ya kujumuisha mambo haya kama yale yanayofaa kujumuishwa kwenye mtihani," alisema Kipsang.
Wakati huo huo, katibu huyo amesema wizara ya elimu inaunga mkono hatua ya wanafunzi kuendesha uchaguzi wa viongozi wao, badala ya viongozi hao kuchaguliwa na walimu, akiongeza kuwa hatua ya wanafunzi kuwachagua viongozi wao inaendelezwa kwa sasa kwenye shule nyingi.
Kulingana naye, baadhi ya wale wanaotaka kuwania nafasi hizo za uongozi huwajuza wanafunzi wenzao kuhusu maono yao, hatua ambayo huwapelekea kuchaguliwa kuwa viongozi.
Hatua hiyo ya kufanya uchaguzi, kwa mujibu wa Kipsang, huwapelekea wanafunzi kukumbatia mfumo wa kufanya uchaguzi, na isitoshe, hatua hiyo inawapelekea wanafunzi hao kutambua kwamba viongozi hao ni wale ambao wamechaguliwa na wenzao.
"Serikali za wanafunzi ni serikali ambazo zimechaguliwa na pia zimechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia. Wanafunzi wataweza kuwajuza wanafunzi wenzao maswala ambayo wamesimamia na maono yao na wanachaguliwa kutokana na hilo. Hii leo, kuna serikali ya kitaifa ya wanafunzi na hilo ndilo tunalohimiza, ili waweze kukuwa wakijua umuhimu wa kupitia shughuli ambayo imekubaliwa na kila mmoja wao," alisema katibu huyo wa elimu.