Wizara ya kilimo, ufugaji na uvuvi Kaunti ya Nakuru ina lengo la kuwapa chanjo dhidi ya ugonjwa wa kimeta zaidi ya mifugo elfu mia nne katika kipindi hiki.
Akizungumza afisini mwake Jumanne, afisa mkuu mtendaji katika wizara hiyo Purity Muritu amesema ya kwamba hatua hiyo itazuia wakulima kupata hasara kutokana na ugonjwa huo.
Kutokana na mvua ambayo inaendelea kushuhudiwa katika eneo hili, na ambapo ugonjwa huo huletwa na kusambazwa na mvua, afisa huyo amesema kuwa kwa kuwachanja mifugo hao, itazuia mifugo katika eneo hilo kuathiriwa.
Chanjo hiyo, ambayo serikali ya Kaunti ya Nakuru inapeana kupitia wizara hiyo haina malipo, afisa huyo amewataka wakulima kujitokeza na kuwapeleka mifugo yao kwa chanjo.
Hadi kufikia sasa Muritu amedhibitisha kuwa wakulima kutoka zaidi ya maeneo bunge sita ya kaunti hiyo, mifugo wao wameweza kuchanjwa.
Hata hivyo Muritu amewataka na kuwashauri wakulima kuwa maakini na wasisafirishe mifugo yao kutoka eneo moja hadi lingine endapo kuna hofu ya ugonjwa wowote hatari wa mifugo, hii ikiwa ni njia mojawapo ya kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo, na badala yake waripoti kwa mafisaa wa afya ya mifugo waliokaribu.