Wakazi wengi kutoka Kaunti ya Kisii wanataka gari aina ya Probox ziondolewe barabarani kwa kusababisha ajali za mara kwa mara.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Alhamisi mjini Kisii, idadi kubwa ya wakazi na abiria, wakiongizwa na Alloys Marucha, waliomba idara ya uchukuzi nchini kuyaondoa magari hayo barabarani kabla hayajagharimu maisha ya wengi.

Mnamo siku ya Jumanne, gari aina ya probox iligonga kijana mmoja na akafariki katika eneo la Nyatieko Kisii na kujeruhi mmoja, huku siku ya Jumatatu gari aina hiyo pia iliwajeruhi watu watatu ilipohusika katika ajali eneo la Miruka.

“Magari haya ya Probox yanahusika katika ajali kila mara katika barabara nyingi, magari hayo si ya kusafirisaha abiria lakini unayapata yakifanya uchukuzi kila siku,” alisema Marucha.

“Pia magari hayo hurundika watu hadi 13, tunaomba idara ya uchukuzi kuyaondoa magari hayo barabarani kwani maisha ya wengi yamepotea kupitia visa vya ajali kila wakati,” aliongeza Marucha.

Ikumbukwe kuwa Idara ya uchukuzi nchini iliyapiga marufuku magari hayo kusafirisha abiria, agizo ambalo limeonekana kupuuzwa hadi sasa haswa katika kaunti za Kisii na Nyamira.

Sasa wizara hiyo ya uchukuzi imeombwa kujaribu kila iwezalo kuhakikisha magari hayo yamepigwa marufuku tena.