Serikali kupitia katika Wizara ya Uchukuzi ikishirikiana na mamlaka ya mambo ya baharini KMA wamezindua mpango wa pamoja wa kuboresha sekta ya uvuvi na huduma za baharini.
Mpango huo utawezesha serikali kuu kushirikiana na zile za kaunti kufanya maamuzi ya pamoja kuhusu maswala yanayogusia bandari, usalama wa majini pamoja na kuboresha sekta ya uvuvi.
Akiongea mjini Mombasa siku ya Jumatano wakati wa uzinduzi huo, katibu katika wizara ya uchukuzi Bi Nancy Karigithu alisema kuwa mpango huo pia utaleta mabadiliko makubwa katika biashara za bandarini.
“Lengo kuu la huu mpango ni kuleta pamoja upande wa serikali, sekta za kibinafsi pamoja na washikadau wote wanaotegemea huduma zinazotolewa kupitia bahari yetu. Tunataka sote tusonge mbele kwa pamoja,” alisema Bi Karigithu.
Katibu huyo pia ameongeza kuwa serikali kuu imeamua kuja na mikakati dhabiti kuangazia kwa kina changamoto zinazoshuhudiwa baharini ikiwa ni pamoja na matumizi bora ya rasilimali muhimu zilizopo.
Kati ya changamoto ambazo zimekuwa zikishuhudiwa ni pamoja na wavuvi kudai kutoshughulikiwa na serikali katika biashara zao, huku wakiongeza kuwa wavuvi wa kigeni wamekuwa wakiendeleza uvuvi humu nchini bila vibali.
Wakati huo huo, katibu huyo alieleza kuwa Kenya iko na fursa ya kuwa na sehemu maalum za kujitengezea boti na meli iwapo mpango huo mpya utatekelezwa ipasavyo, na kutaja sekta ya utalii kama inayolengwa zaidi.
Bandari ya Mombasa hutegemewa sana na watu wengi kiuchumi kutokana na nafasi za kazi pamoja na biashara mbalimbali zinazoendeshwa sehemu hiyo.