Jamii ya watu wanaoishi na ulemavu wa ngozi (zeruzeru) katika eneo la Pwani imeilaumu serikali kwa kukosa kukosa kuwahusisha katika maswala ya maendeleo.
Jamii hiyo, ikiongozwa na mwakilishi wao Alphonce Ngowa, ililalamikia kutengwa na kutohusishwa vyema katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumza wakati wa kongamano la kiuchumi mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Ngowa alisema kwamba jamii hiyo imeonekana kusaulika katika maswala mengi ya kimaendeleo na kiuchumi.
“Serikali imeonekana kuitenga jamii ya walemavu wa ngozi katika maswala mbalimbali ya kimaendeleo mashinani, na hata wakati wa kuimarisha uchumi wa nchi. Jamii hii ina uwezo wa kuibadili taifa hili kimaendeleo, na tunaomba viongozi wa serikali kutuhusisha katika miradi mbalimbali ya Maendeleo,” alisema Ngowa.
Jamii hiyo imeitaka serikali kuweke mikakati ya kuhakikisha kuwa inawatengea bajeti maalum ya kutekeleza miradi midogo midogo ya maendeleo mashinani ili waweze kujiendeleza kuichumi.
Wakati huo huo, Ngowa aliwataka magavana wa kaunti za pwani hasa kupitia muungano wa jumuiya ya kaunti za pwani, kujenga shule maalum ya watu walio na ulemavu ili kuwawezesha wale wanaopitia changamoto za kimazingira kupata fursa ya kupata elimu.