Ikulu ya Rais imesema kuwa zaira ya Rais Uhuru Kenyatta katika eneo la Pwani sio ya kisiasa bali ya kutekeleza ajenda za serikali nchini.
Msemaji wa Ikulu ya Rais nchini Manoah Esipisu amesema kuwa shughuli ambazo Rais Kenyatta anatekeleza katika ukanda wa Pwani katika ziara hiyo ni kati ya ahadi ambazo serikali ya Jubilee iliahidi kwa wakenya wakati wa uchaguzi mkuu uliyopita na sharti ahadi hizo kutimizwa.
Kwenye kikao na wanahabari katika Ikulu ya Rais mjini Mombasa siku ya Jumatano, Esipisu alisema kuwa uvumi unaoeneza na baadhi ya viongozi wa kisiasa wa mrengo wa upinzani ni njia za kujipatia umaarufu wa kisiasa na serikali kwa sasa haina mipango ya kufanya kampuzi za kisiasa mapema bali kukamiliza ahadi ilizotoa kwa wakenya.
"Ziara ya Rais Kenyatta eneo la Pwani sio ya kisiasa bali yuko Pwani kutekeleza ajenda za serikali pamoja na kutimiza ahadi serikali ilitoa kwa wakenya wakati wa uchaguzi kwa hivyo tusipotoshwe na baadhi ya watu fulani kwa lengo za kuleta uhasama, rais yuko Pwani kuhakikisha kuwa ajenda zote za maendeleo na ukuzaji uchumi unatimizwa," alieleza Esipisu.
Amesema kuwa serikali imejitolea kikamilifu kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha kuwa maswala ya kimaendeleo, uchumi, usalama, utalii na muundo msingi yanatekelezwa kwa manufaa ya wakenya.
Kauli ya Ikulu ya Rais imejiri baada ya mrengo wa upinzani Cord kudai kuwa shughuli ambazo Rais Kenyatta anatekeleza katika ukanda wa Pwani ikiwemo utoaji wa hati miliki za ardhi kuwa njama ya kujipigia debe kisiasa ili serikali ya Jubilee kurejea madarakani.