Share news tips with us here at Hivisasa

Muungano wa vijana kwa jina ‘ Yes We Can’ katika Kaunti ya Kisii umekosoa ziara ya viongozi wa kaunti hiyo ambao walisafiri hadi Eldoret kwa naibu Rais William Ruto kwa kile walichodai ni utumizi mbaya wa pesa za umma.

Hii ni baada ya viongozi wa Kaunti za Kisii na Nyamira, wakiongozwa na naibu gavana wa Kaunti ya Kisii Joash Maangi kusafiri Eldoret kwa William Ruto siku ya Alhamisi, na kusema hiyo ni utumizi mbaya wa pesa za umma ambazo zingefaa kuleta maendeleo kwa kaunti hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Alhamisi mjini Kisii, kiongozi wa muungano huo wa vijana Denis Orioki alikosoa ziara hizo ambayo ilisemekana kuwa ya kisiasa wala sio maendeleo jinsi walivyodai hapo mapema kabla ya kufunga safari hiyo.

Kulingana nao, mkutano huo ungekuwa wa maendeleo ungefaa kuandaliwa katika eneo la Gusii na sio Eldoret jinsi ilivyofanyika, na kusema huo ni uharibifu wa pesa za umaa za kufanya maendeleo.

“Imeonekana kuwa baadhi ya viongozi wa Kaunti ya Kisii wameanza kutumia pesa za umma vibaya, haya mamilioni ya pesa yaliyotumika kwa ziara ya Eldoret yangefaa kuleta maendeleo hapa Kisii,” alisema Orioki.

Ziara hiyo ilihusisha wabunge 10 kutoka kaunti hizo mbili na baadhi ya wawakilishi wadi.

Matamshi hayo yaliungwa mkono na mbunge wa Mugirango kusini Manson Nyamweya, mbunge wa Bomachoge Chache Simon Ogari, seneta wa Kaunti ya Kisii Chris Obure na Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae na kusema mkutano huo hukuwa wa maendeleo ila wa siasa tupu.