Waumini wa Kanisa Katoliki jimbo la Kisii ambao wangependa kuhudhuria misa itakayoongozwa na Papa Francis wameombwa kutuma majina yao pamoja na nambari ya vitambulisho haraka iwezekanavyo kwa Idara ya uchungaji iliyoko katika afisi za jimbo mjini Kisii.
Kasisi Edward Mokano anayeshirikisha shughuli za uchungaji katika jimbo alisema hili litawezesha afisi yake kutoa vitambulisho maalum ambavyo vitawapa fursa ya kuingia katika Chuo kikuu cha Nairobi ambapo misa hiyo itaandaliwa na maeneo mengine yaliyotengwa kwa shughuli hiyo.
Akizungumza katika kanisa katoliki la mtakatifu Yosefu Kisii siku ya Jumanne, kasisi huyo aliwataka waumini hao kuwasilisha orodha hiyo kupitia kwa makasisi wanaosimamia parokia zao ili vitambulisho hivyo viweze kuwafikia kwa haraka.
“Kutokana na mikakati kabambe ya kiusalama iliyowekwa na serikali katika juhudi za kumpokea kiongozi huyo wa kanisa katoliki duniani, hakuna atakayeruhusiwa kuingia sehemu zilizotengwa bila kitambulisho hicho maalum,” alisema Kasisi Mokano.
Pia aliwashauri wanaotaka kuhudhuria misa hiyo kusafiri hadi Nairobi mapema akisema milango itafunguliwa kati ya saa kumi na mbili na saa moja asubuhi huku kila mmoja akitarajiwa kuwa amekaa kufikia mwendo wa saa mbili.
Kasisi huyo alisema baba mtakatifu atakutana na vijana katika ziara yake humu nchini na kuwasihi vijana kutoka jimbo hilo kujitokeza ili waweze kukutana na Papa Francis ambaye huvutiwa sana na shughuli za vijana.