Yamekuwa ni mazoea kwa wahudumu wa matatu kupandisha nauli bila utaratibu wakati wateja wanapoongezeka.
Wakati huu ambapo shule zinafungwa, biashara hiyo imewanogea wahudumu wa Matatu ambao wameanza kuongeza nauli katika maeneo mbalimbali nchini.
Kufikia siku ya Jumatano jioni, wasafiri kwenye barabara ya kutoka Kisiani kwenda Bondo walianza kulazimika kulipia nauli isiyokuwa ya kawaida, baada ya wanafunzi kuanza kumiminikia usafiri.
Abiria kwenye barabara hiyo walitaka wenye Matatu kuzingatia nauli ya kawaida kwa kila msimu na kwenda na mabadiliko ya uchumi wakati bajeti inaposomwa.
Walisema kwamba nauli inafaa kupanda iwapo bei ya petroli na diseli imetangazwa kupanda nchini.
''Hatuelewi ni kwa nini wenye Matatu wanapenda kuongeza nauli bila kufuata utaratibu wowote. Hali hiyo inatudhulumu sisi abiria wa kila siku kwenye barabara hili,'' alisema Maurine Amolo aliyeongea na Mwandishi huyu wa habari mnamo siku ya Alhamisi.
Aidha, wafanyibiashara wanaoendesha biashara yao mjini Kisumu na wanatoka katika maeneo ya Seme, Akala na mengineyo kwenye barabara hiyo kuelekea Bondo walisema hali hiyo inawaathiri sana kiuchumi.
Pia walitaka vyombo husika kuwajibika kwa kuingilia kati na kuwasaidia wakati hali kama hiyo inapotokea.