Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwenyekiti wa Maendeleo ya Wanawake katika Kaunti ya Kisii Bathseba Zanayo amewaomba akina mama kujiunga na vikundi vya maendeleo ili wapate mikopa ambazo zitawasaidia katika miradi mbali mbali.

Akiongea siku ya Alhamisi katika uwanja wa Nyamache, eneo Bunge la Bobasi katika Kaunti ya Kisii katika hafla ya kukagua maendeleo katika eneo hilo, mwenyekiti Zanayo alisema kujiunga na vikundi ndio njia ya kupata mikopo kwa wakina mama na ni vyema waanze kuviunda au kujiunga.

Aidha, alisema kuwa akina mama ndio wana jukumu kubwa la kuinua uchumi wa kaunti kwa kuwa wao hufanya kazi ngumu ya kuhakikisha maendeleo yamenawiri katika jamii na kuwaomba viongozi kuwasaidia akina mama ili nao waweze kunufaika na kujiendeleza kimaisha.

“Nawaomba akina mama wote kujiunga katika vikundi mbali mbali ili nasi tuweze kujiendeleza kimaisha na kuinua uchumi wa kaunti yetu kwa kuwa ni sisi wenyewe ndio tuna jukumu la kuinua viwango vya maendeleo,” alihoji Zanayo.

Mwenyekiti huyo alisema vikundi vya maendeleo ni muhimu kwa akina mama kwani ndio nguzo ya kuwasaidia kuinua miradi ambayo wanaanzisha.

Kwingineko, alipongeza serikali ya Kaunti ya Kisii kwa kuwakumbuka na kusema wataendelea kushirikiana na serikali hiyo ili kuinua uchumi wa kaunti hiyo.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwa na wanaosimamia idara mbali mbali katika Kaunti hiyo.