Kina mama kutoka kaunti ya Nyamira wameombwa kujisajili kupokea pesa zinazopeanwa na serikali ili kuwasaidia kuimarisha biashara zao.
Kulingana na mwakilishi wa kina mama kwenye kaunti hiyo Alice Chae, aliyekuwa akiongea na akina mama kwenye maeneo mbalimbali siku ya Jumatatu, serikali ya kitaifa imetenga pesa nyingi kwa minajili ya kuendeleza akina mama. huku akiwaomba kubuni miradi itakayofadhiliwa na pesa hizo.
"Serikali ya kitaifa imetenga pesa nyingi kwa minajili ya kuendeleza akina mama, na ninawaomba kina mama kubuni miradi inayoweza kufadhiliwa na pesa hizo," alisema Chae.
Chae alisema kuwa iwapo kina mama watapokea pesa hizo pasina shaka maisha yao yataimarika huku akiongeza kusema kuwa serikali imeweka mikakati kabambe kuimarisha maslahi ya kina mama.
"Iwapo kina mama watapokea pesa hizo pasina shaka maisha yao yataimarika na serikali imeweka mikakati kabambe ya kuwasaidia akina mama kuimarisha maisha yao," alihoji Chae.
Mwakilishi huyo wa kina mama kwenye bunge la kitaifa aidha alisema kuwa akina mama wa taifa hili wamepewa nafasi ya kikatiba na yafaa waitumie vizuri kustawisha maisha yao, na akaongezea kuwa kina mama wanafaa kuwa kwenye mstari wa mbele kutuma maombi ya nafasi za kazi kwenye nyadhifa za uongozi.
"Katiba ya Kenya inatambua haki za akina mama na inastahili watumie uhuru huo vizuri kustawisha maisha yao, na inafaa kina mama hao wawe kwenye mstari wa mbele kutuma maombi ya nafasi za kazi za nyadhifa mbalimbali," alisema Chae.