Share news tips with us here at Hivisasa

Balozi wa Denmark humu nchini Mette Knudsen ametoa wito kwa serikali kuwapa nafasi wanaharakati pamoja na mashirika ya kutetea haki za binadamu kutekeleza shughuli zao bila kutatizwa na vyombo vya usalama.

Akizungumza katika hafla moja mjini Mombasa wakati alikuwa na kikao na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu pamoja na viongozi mbali mbali wa mashirika ya kijamii siku ya Alhamisi, Mette alisema kuwa kila mmoja ana nafasi ya kutekeleza haki ambazo zimetungwa katika katiba.

Aidha, aliongezea kuwa ni sharti mashirika hayo yapewe heshima na nafasi kufanya kazi zao, ikizingatiwa kuwa wanatekeleza wajibu muhimu wa kuwatetetea wanyonge na kuweka wazi mambo ambayo serikali haijui au haijaangazia.

Aliwashauri wanaharakati hao pia nao kuwa katika mstari wa mbele kufwata sheria wanapofanya kazi zao ili kujiepusha na mtafaruku na serikali iliyoko mamlakani.

Balozi huyo alisema kuwa serikali yake itaendelea kufanya juhudi kuona kuwa haki za kila mtu zinatetewa, na kudokeza kuwa kupitia ubalozi huo, serikali ya nchi yake itaendelea kutoa msaada kwenye nchi ya Kenya unapohitajika, na kuwasihi viongozi wa mashirika hayo kusimama imara na kuwajibikia nafasi ya kutetea jamii.

Mashirika mengi kutoka kote nchini Kenya, hasa yale ya kutoka eneo la pwani yamekuwa yakilalamikia kunyanyaswa na serikali kuu hata baadhi yao kufungiwa akaunti zao hata wakati mmoja mengine kuhusishwa na shughuli za uharamia na ugaidi.