Share news tips with us here at Hivisasa

Wakaazi wa wadi ya Bahati haswa kituo cha kibiashara cha Maili Kumi, wamefurahishwa na hatua ya serikali ya kaunti ya Nakuru kufungua barabara moja ambayo ilikuwa imenyakuliwa.

Barabara hii inaunganisha mashamba manane ya ekari mbili katika kila upande, na ilikuwa imefungwa tangu mwaka wa 1984 katika kituo hicho cha kibiashara. Barabara hiyo sasa inahudumia zaidi ya watu 100 kutoka eneo hilo.

Akidhibitisha hayo, mwakilishi wa wadi ya Bahati kwenye bunge la kaunti ya Nakuru Peter Nderitu Mwangi amesema kwamba jumla ya wakaazi 42 ndio walitia saini ombi la kutaka serikali ya kaunti iingilie kati na kufungua barabara hiyo. Hii ilikuwa ndio waache kuzunguka mbali wakati wanatafuta huduma katika kituo cha kibiashara cha Maili Kumi, ikiwemo za afya.

“Waliandika majina yao na wakatia saini, nasi tukafuatilia jambo hilo japo kulikuwa na siasa nyingi kwani aliyekuwa ameifunga alikuwa akikingiwa kifua na watu fulani,” akasema bwana Nderitu.

“Sasa tunamwaga changarawe eneo hilo ili isiharibike mvua ikinyesha, na hii ni dhihirisho kwamba kaunti ya Nakuru hatutavumilia unyakuzi wa mali ya umma,” aliongeza Nderitu.

Majuma kadhaa yaliyopita, akizungumza mjini Naivasha, mwenyekiti wa tume ya ardhi nchini NLC Mohamed Swazuri, alilaumu serikali ya kaunti ya Nakuru chini ya gavana Kinuthia Mbugua akisema haishirikiani na tume hiyo katika kusuluhisha matatizo yanayokumba barabara zinazoelekea ziwani Naivasha ambazo zimefungwa na wanyakuzi.