Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mbunge wa Kitutu Masaba Timothy Bosire amemuomba Rais Uhuru Kenyatta kujumuisha viongozi wote katika idara ya usalama ili kupambana na ukosefu wa usalama nchini.

Akiongea mnamo siku ya Alhamisi katika eneo la Nyangori wakati alitoa pesa za ujenzi wa kituo cha polisi katika eneo hilo, Bosire, ambaye ni mwekahazina katika chama cha ODM alisema kuwa Rais Kenyatta hajawajumuisha viongozi wa mlengo wa CORD kupambana na ukosefu wa usalama nchini.

“Sisi tukiwa viongozi wa muungano wa upinzani na wale wa serikali, sote ni viongozi, tunahitaji kukaa pamoja na kufanya kazi ya kuridhisha na huo ndio mwelekeo kamili ambao unastahili upatikane katika nchi yetu,” alidokeza Bosire.

“Hadi sasa, Rais amekuwa akisitasita kati ya upinzani na serikali, tunataka kumwahakikishia kwamba sote tukiwa viongozi tunataka nafasi kamili ili tuongee pamoja na tupate usalama wa nchi yetu,” aliongeza Bosire.

Aidha, Bosire alisema umoja wa viongozi katika nchi ya Kenya utaendeleza nchi mbele na vijana watapata ajira.

Wakaazi nao walifurahishwa na matamshi ya mbunge huyo, huku wakisema viongozi wote wajumuishwe katika idara ya usalama ili kupambana na visa vya ukosefu wa usalama.