Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Bunge la Kaunti ya Uasin Gishu lililazimika kusitisha shughuli zake za siku ili kujadili kwa dharura hoja ya usalama.

Hoja hiyo iliwasilishwa bungeni humo na kiongozi wa wachache Ramadhan Ali siku ya Jumatano.

Ali ambaye ni mwakilishi wa wadi ya Kiplombe alisema matukio ya mauaji ya kiholela mjini Eldoret yameongezeka kwa idadi kubwa hivi majuzi.

Akiwasilisha hoja hiyo bungeni, Ali alisema namna matukio hayo yanavotokea inaashiria kwamba yanapangwa na kutekelezwa na kundi fulani.

Akirejelea mauaji ya hivi maajuzi katika mtaa wa Maili Nnne, Ali alitaka bunge kutoa agizo kwa idara ya usalama katika Kaunti ya Uasin Gishu kuchunguza mauaji hayo na kuwasilisha ripoti kwa bunge hilo.

“Serikali ya kaunti na serikali kuu ni sharti washirikiane kuimarisha usalama,” alisema Ali.

Mwakilishi huyo alisema matukio hayo yamefanya watu mjini Eldoret waishi kwa uoga ambapo wafanyibiashara kwa sasa wamelazimika kufunga biashara zao mapema.

Kulingana na Ali, iwapo hoja hiyo itapewa umuhimu unaostahili na bunge hilo, visa vya kudorora kwa usalama vitadididmia.

Kiongozi wa shughuli katika bunge hilo Bw Josphat Lowoi alitaka kupewa muda zaidi ili kujadiliana na vitengo vya usalama na kutoa ripoti kamili baadaye bungeni humo.

Spika wa bunge hilo Bw Isaack Terer aliamuru Bw Lowoi kuwasilisha ripoti kamili bungeni humo siku ya Alhamisi wiki kesho kuhusiana na hali hiyo ili bunge litoe kauli yake.