Share news tips with us here at Hivisasa

Kinara wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi ametoa wito kwa bunge la kitaifa na taasisi zinazohusika na usimamizi wa rasilimali za umma kuunda sheria zitakazothibiti utumizi mbaya wa fedha za umma.

Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatatu, baada ya kukutana na baadhi ya viongozi wa Kiislamu, Mudavadi alisema kuwa bunge lina jukumu la kutafuta suluhu ya ufujaji wa fedha katika afisi mbali mbali za serikali badala ya kujikita katika mijadala ya malumbano isiyokuwa na manufaa kwa umma.

“Ripoti kutoka kwa mhasibu mkuu wa serikali pamoja na msimamizi wa bajeti ya kitaifa zinaonyesha wazi utumiaji mbaya wa raslimali za umma ilihali wabunge wanashindwa kuangazia masuala kama hayo,” alisema Mudavadi.

Kauli hii inajiri kufuatia malalamishi kuwa serikali haina fedha haswa baada ya kucheleweshwa kutolewa kwa fedha za kuendesha serikali za kaunti pamoja na kulemaa kwa shughuli za bunge ikiwemo kukatwa kwa umeme katika majengo ya bunge.

Aidha, katika kikao hicho, Mudavadi alizungumzia suala la misimamo mikali miongoni mwa vijana kwa kusema kuwa vita dhidi ya itikadi kali hazipaswi kuelekezwa kwa dini fulani.