Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwenyekiti wa chama cha walimu nchini Knut tawi la Masaba Kusini katika Kaunti ya Kisii Meshack Aiko Obonyo amewataka wanasiasa kukoma kuwatumia walimu wakati wa uchaguzi tu.

Akiongea katika eneo la Wadi ya Gesusu kwenye mazishi ya Lazurus Ombaki aliyekua afisa mstaafu wa magereza humu nchini na nduguye mwanasiasa Hezekiel Ombaki wa Nyaribari Masaba, mwenyekiti Obonyo kemea tabia ya wanasiasa ambao hua wanaomba usaidizi wa walimu wakati uchaguzi unapokaribia na hatimaye kupotea pindi tu wanapochaguliwa kama viongozi na kurudi baada ya miaka mitano kuwarai bila kuwakumbuka walimu hao wanapokuwa na shida.

"Tumekuwa na vita kuhusu mishahara yetu kama walimu na hamna mwanasiasa kutoka eneo hili letu la Masaba ambaye amewahi kusimama nasi wakati huo wa kunyanyaswa na kulilia haki zetu kama walimu, basi ngojea uchaguzi ujao mtawaona walimu pia vile watawapa mgongo,'' alisema Obonyo.

Aidha, mwenyekiti huyo alisema kuwa chama chao cha Knut hakitalala hadi pale serikali kuu itawapa haki zao. Alisema pia walimu wapo tayari kugoma kama serikali na wakuu wa chama chao Knut, wakiongozwa na bwana Wilson Sossion hawataweza kuelewana kuhusu nyongeza ya mshahara yao.

"Tupo tayari kwa vyovyote vile sasa hatutishiki tena na serikali kuu, pia serikali zetu za kaunti zinafaa kuwapa mkono walimu kupata haki zao ili nasi kama walimu tuwe na roho safi ya kusaidia watoto wetu," alisema bwana Evans Kalulu Bonuke, mwekahazina wa tawi hilo, aliyehudhuria hafla hiyo ya mazishi.

Pia bwana Bonuke alisema walimu na vijana ndio wanaongoza kuwa na kura nyingi katika eneo hilo na kote nchini.