Hatimaye chanjo dhidi ya ugonjwa wa kupooza (Polio) katika Kaunti ya Kisumu ilianza vyema kama ilivyopangwa awali.
Baada ya kampeni ya wiki mzima iliyofanywa na maafisa wa afya katika kaunti hiyo kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa chanjo hiyo, juhudi hizo zilionekana kufaulu wakati wananchi walipojitokeza kushiriki zoezi hilo mnamo siku ya Jumapili.
Madakitari wanaoendesha shughuli hiyo katika Kaunti ya Kisumu walizuru makanisa ya eneo hilo huku wakipata kazi rahisi wakati wazazi walipotoa wanao walio na umri wa chini ya miaka mitano kupata chanjo.
Awali uoga ulikuwa umetanda miongoni mwa maafisa hao ambao walidhania baadhi ya wananchi wangelisisia zoezi hilo kutokana na semi zilizotoka vinyani mwa wengi kukashifu chanjo hiyo, baada ya kanisa katoliki nchini kutaka wananchi kukataa chanjo hiyo kwa kile walichodai kuwa ina madhara ya kiafya.
Baadhi ya waliojitokeza siku ya Jumapili walisifia chanjo hiyo wakisema kuwa ni ya muhimu kwa afya ya baadaye ya watoto wao.
Pauline Adikinyi ambaye pia wanawe wawili walipata chanjo aliwaambia Waandishi wa habari kuwa mzazi anayejali maisha ya mwanawe atazingatia, atajitokeza kushiriki zoezi hilo ikizingatiwa kuwa wengi wanashuhudia visa vya watu kupooza hata kisha kuwa na umri mkubwa, kwa kuwa walikosa chanjo hiyo utotoni.
''Mimi mtoto wangu hawezi akakosa chanjo hii kwa kuwa nafahamu kwa ndani faida zake,'' alisema Adikinyi.