Share news tips with us here at Hivisasa

Naibu Gavana wa Kaunti ya Uasin Gishu, Daniel Chemno, amedai kuwa ufisadi umekita mizizi katika tawi la Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) tawi la Eldoret.

Akihutubia waandishi wa habari afisini mwake siku ya Alhamisi, Bw Chemno alidai kuwa ufisadi huo ulichangia kutoweka kwa zaidi ya lita 100,000 za mafuta yalionaswa yakiwa mikonono mwa matapeli.

Mafuta hayo yalinaswa katika eneo la Juakali mwishoni mwa mwaka jana ambapo Bw Chemno alidai kuwa maafisa wa KRA walikosa kushirikiana na vitengo vingine kubaini yalikotoka mafuta hayo.

“Maafisa wa polisi waliponasa mafuta haya tuliita maafisa wa KRA ili wabaini yalikotoka mafuta hayo na kule yalikokuwa yakipelekwa, lakini walikataa kushirikiana nasi,” alisema Chemno.

Bw Chemno alisema kujitenga kwa maafisa hao kuliashiria kuwa kulikuwa na ufisadi katika tukio hilo.

Hata hivyo, Afisa mkuu wa KRA North-Rift Bi Florence Atori alitetea shirika lake huku akitaka wadau wote kushirikiana ili kukabiliana na ufisadi katika sekta ya mafuta.

“Hakuna haja ya kulaumu KRA pekee. Hata utawala wa kaunti na wadau wengine wana majukumu ya kutekeleza katika vita dhidi ya ufisadi na ukwepa kulipa Ushuru,” alisema Bi Atori

Kwa upande wake naibu gavana huyo alidai kuwa ufisadi unaoendelezwa na KRA unafanya serikali kupoteza mamilioni ya pesa za ushuru katika kaunti za North-Rift.

“Haya mafuta yamesababisha kupotea kwa zaidi ya Sh10m ambapo serikali ingepata ushuru wa aslimia 40 wa pesa hizi,” alisema Chemno.

Kiongozi huyo alisema uchunguzi uliofanyiwa mafuta hayo ulibaini kuwa yalikuwa ya kuuzwa katika nchi za kigeni kabla ya kubadilishwa na kuchanganywa na mafuta taa ili yauzwe na matapeli humu nchini.

Naibu gavana huyo alitaka maafisa wa KRA katika tawi hilo kuchukuliwa hatua za kisheria.