Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Naibu Gavana wa Kaunti ya Uasin Gishu Daniel Chemno amewahimiza viongozi kote nchini kushirikiana na dini zote ili usalama uimarishwe nchini.

Naibu gavana huyo alikuwa akizungumza baada ya kutoa mchango wa chakula wa zaidi ya shilling elfu 30 kama msaada wa kuwasaidi wasiojiweza wakati wa sherehe ya Eid-al-fitr.

Akizungumza na wanahabari katika msikiti wa Jamia mjini Eldoret siku ya Alamisi, naibu gavana huyo alisema kuwa wao kama wakazi wa kaunti wanashirikana bila ubaguzi wa dini au jamii.

“Sisi sote ni watu wa jamii moja. Hakuna mwisilamu au mkristo, ni muhimu kushirikiana kuleta amani nchini,”alisema Chemno.

Chemno alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na vitengo vya usalama ili kukabiliana na utovu wa usalama nchini hasa wakati wa sherehe hizi.

Hata hivyo, Chemno aliwapa viongozi wa kidini changamoto ya kushirikiana na serikali kupiga vita pombe haramu.

Sheikh Mohammed Husein, Imam wa msikiti wa Jamia alipongeza serikali ya kaunti kwa kuonyesha heshima kwa dini tofauti katika kaunti hiyo.

“Ingawa kuna magaidi kule nje wanaojaribu kuharibu jina la kiislamu, sisi kama wakazi wa Uasin Gishu tutashirikiana kuangamiza ugaidi,” alisema Husein.

Husein aliahidi kuwa watashirikiana na vikosi vya usalama kuangamiza ugaidi nchini.