Kiongozi wa walio wengi bungeni ambaye pia ni mbunge wa Garissa mjini Aden Duale, amekashifu Waziri wa Elimu Jacob Kaimenyi kwa kutaka mitihani ya kitaifa ihairishwe katika maeneo ya Kaskazini Mashariki.

Share news tips with us here at Hivisasa

Eneo hilo limekuwa na changamoto nyingi hasa katika sekta ya elimu kufuatia utovu wa usalama na mashambulizi ya kigaidi, hali iliyopelekea walimu wengi kuhama maeneo hayo.

Duale aliyekuwa akizungumza siku ya Jumatano mjini Garissa alisema kuwa wanafunzi wote wa kidato cha nne na darasa la nane ni sharti wafanye mitihani yao ya kitaifa mwaka huu.

Duale aliongeza kuwa hatua ya kuhairisha mitihani hiyo itawaathiri wanafunzi kimasomo na kuwa wanafunzi wa maeneo hayo tayari wamejitayarisha vyema licha ya changamoto zilizoko.

"Wanafunzi hao waachwe wafanye mtihani wa kitaifa kwani tayari wamejitayarisha vilivyo,” alisema Duale.

Wito wa waziri huyo wa elimu ulisababishwa na ukosefu wa walimu ulioshuhudiwa katika maeneo hayo na ulilenga kuwapa wanafunzi muda zaidi wa kujitayarisha.